Azerbaijan imesema wanajeshi wake 2,783 waliuwawa katika vita vilivyosababishwa na mgogoro kati yake na wanajeshi wa Armenia wa kuwania kulidhibiti jimbo la Nagorno Karabakh.

Nchi hiyo pia imesema wanajeshi wake zaidi ya 100 bado hawajulikani waliko hii ikiwa ni mara ya kwanza Azerbaijan kutangaza idadi ya wanajeshi wake iliyowapoteza kutokana na mgogoro huo uliozuka mwezi Septemba na kumalizika mwezi uliopita baada ya kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita yaliyosimamiwa na Urusi.

Maeneo kadhaa yaliyokuwa awali yakidhibitiwa na Waarmenia yalikabidhiwa Azerbaijan ambayo wanajeshi wake waliyateka ikiwemo yale waliyoyapoteza mwanzoni mwa vita vya miaka ya 1990.

Armenia bado haijatangaza idadi ya mwisho ya wanajeshi wake waliouwawa ingawa wizara ya afya ya nchi hiyo ilithibitisha mwezi Novemba kwamba wanajeshi wake 2,317 waliuwawa.

Taarifa nyingine zinasema rais Recep Tayyip wa Erdogan wa Uturuki ambaye ni mshirika mkubwa wa Azerbaijan ataitembelea nchi hiyo kuanzia Desemba 9 hadi 10.

Ziara hiyo itakuwa ya kwanza ya kiongozi wa kigeni nchini Azerbaijan tangu kusitishwa kwa vita wiki sita zilizopita.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Desemba 4, 2020
Rapa Casanova mikononi mwa FBI