Aliyewahi kuwa Mfadhili wa Klabu ya Simba SC Azim Dewji amesema mchezo wa Watani wa JADI kati ya Young Africans na Simba SC hautabiriki, hivyo kwa upande wake anaamini yoyote anaweza kuibuka kidedea.
Miamba hiyo ya Soka la Bongo itapambana katika mchezo wa mzunguuko wa 21 wa Ligi Kuu msimu huu kesho Jumamosi (April 30) Uwanja wa Benjamin Mkapa, saa kumi na moja jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Azim ambaye aliiwezesha Simba SC kufika Hatua ya Fainali Kombe la CAF mwaka 1993 na kufungwa dhidi ya Stella Abidjan ya Ivory Coast, amesema amekua na uzoefu na michezo ilitozikutanisha timu hizo na ameona mambo mengi tofauti na ilivyotarajiwa na Mashabiki/Wanachama wa pande zote mbili.
Hata hivyo Azim amesema upande wa kiufundi Simba SC ipo vizuri kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi (April 30), na timu hiyo inapaswa kushinda li kuondoa dhana ya Young Africans kutawazwa Mabingwa kabla ya msimu huu 2021/22 haujafikia ukingoni mapema mwezi Juni.
“Kiufundi Simba SC ipo vizuri na inatakiwa kushinda mchezo wa kesho Jumamosi, lakini Soka mara nyingi huwa halitabiriki kwa sababu timu inaweza kuwa vizuri lakini ikapoteza mchezo, na timu inaweza kuwa vibaya ikapata alama tatu za mchezo huo.”
“Kutabiri mchezo wowote unaozikutanisha Simba SC na Young Africans ni zoezi gumu sana, lakini msimu huu Young Africans imeonyesha kuwa vizuri na kocha wao ameisuka timu yake vizuri na pia Mashabiki/Wanachama wameona tofauti kubwa kwenye timu yao, kwa sababu siku za nyuma ilikua ikicheza soka la kubutua butua.”
“Kwa hiyo Soka la kesho In Shaa Allah litakua zuri lakini matokeo ni vigumu sana kuyatabiri, kwahiyo mimi ninashindwa kusema lolote kwa sababu nina uzoefu wa muda mrefu na timu hizi zinapokutana, lolote linaweza kutokea.”
Young Africans kesho itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 54 ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Simba SC inayotetea ubingwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo huo, ikiwa na alama 41, ambazo zinaifanya kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya Young Africans.