Wajumbe wa mkutano wa hali ya hewa uliofanyika nchini Kenya, umeidhinisha Azimio la Nairobi kuwa mkakati wa pamoja na msimamo wa Afrika, kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa na kuwa msingi wa mazungumzo ya mkutano wa COP28 utakaofanyika Dubai mwezi Novemba, 2023.
Katika Mkutano huo wa jijini Nairobi, Marais wasiopungua kumi na watano kutoka nchi mbalimbali barani Afrika, walihudhuria sambamba na Watunga sera, Viongozi wa Serikali, Watoa maamuzi, Wanasayansi, Mashirika ya Kimataifa, Mashirika ya Kiraia na Sekta binafsi.
Aidha, lengo la Mkutano huo lilikuwa ni kufanikisha nguvu za pamoja za kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa na kutoa ufadhili unaohitajika, wa kuimarisha nguvu za kijamii kuzikabili athari za mabadiliko hayo na mishtuko mingine.
Viongozi wa Afrika, wadau mbalimbali, zikiwemo Serikali, Sekta Binafsi, Benki za Kimataifa na Wahisani, wametoa ahadi ya kuchangia jumla ya dola bilioni 23 za Kimarekani, ILI kufadhili ukuaji wa kijani, kupunguza na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa, barani Afrika.