Wadau wa soka wameweka wazi mambo yaliyomfanya kiungo wa Young Africans, Stephane Aziz Ki msimu uliopita kushindwa kufanya vizuri na kuwaka msimu huu.
Aziz Ki ni moja ya sajili zilizotikisa msimu uliopita akitambulishwa saa sita usiku na kuteka mioyo ya wana Young Africans, lakini hakuweza kufanya vyema na kujikuta akianzia benchi katika michezo mingi.
Aliyewahi kuwa kocha wa Young Africans, Charles Mkwasa amesema kuwa staa huyo aliyetokea ASEC Mimosas ana uwezo mkubwa na wa hali ya juu, lakini tatizo alipokuja upepo ulikuwa haujamkubali.
Mkwasa amesema mchezaji huyo ana mambo mengi yanayoweza kumfanya awe bora au asiwe bora katika mazingira mapya, akiyataja mambo kuwa ni mazingira, kocha anayemfundisha, wachezaji aliowakuta kikosini sambamba na muunganiko na wenzake.
“Hizo ni sababu zinazomfanya mchezaji kubadilika. Mfano huyo Aziz Ki wakati alipokuja Young Africans ilikuwa chini ya Nasreddine Nabi na sasa Miguel Gamondi. Huenda aliyeondoka alikuwa hamuelewi kama huyu aliyekuja na ndio maana kawa bora.” amesema kocha huyo.
“Mazingira na ligi ya Tanzania hakuielewa mwanzo, lakini kwa sasa ameielewa na ndio maana ubora uliowafanya Young Africans wamsajili na kuuteka usajili ndio unaanza kuonekana.”
Mkwasa amesema yapo mambo mengi yanayomfanya mchezaji kukosa ubora au kuongezeka, hivyo akipewa muda kama hakuwa vizuri anajiongeza na kwa kujituma na kuongeza jitihada binafsi.
Kocha wa zamani wa Simba SC Abdallah ‘King’ Kibadeni, amesema michezo ambayo nyota huyo amecheza mpaka sasa kafunga na kama hajafunga kachangia upatikanaji wa ushindi.
“Mechi chache tu kaonyesha nini anacho, zikiendelea atazidi kuwa mzuri zaidi, anapambana hakati tamaa na sasa kocha amemuamini na kumpa nafasi,” amesema Kibadeni.
Katika mchezo wa kwanza wa ufunguzi wa Ligi Kuu Bara dhidi ya KMC ambao Young Africans ilishinda mabao 5-0 alifunga bao moja huku ule wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na ASAS katika ushindi wa mabao 2-0 alifunga bao la kwanza ma kuonyesha kiwango bora uwanjani.
Mchezo wa marudiano ambao Young Africans ilishinda mabao 5-1 alihusika katika bao la pili lililofungwa na Wontah Konkoni.