Abiria wa ndege iliyokuwa inataka kuanza safari kutoka jijini Manchester, Uingereza kuelekea jijini Islamabad, Pakistan, amezua taharuki baada ya kufungua mlango wa dharura akidhani ni mlango wa choo wakati ndege ikijiandaa kuruka.
Ndege hiyo inayomilikiwa na Shirika la Ndege la Pakistan ililazimika kuchelewa kwa takribani saa saba kutokana na tukio hilo.
Abiria arobaini waliokuwa ndani ya ndege hiyo waliondolewa kwa muda ili kupisha mafundi waweze kurejesha mifumo katika hali ya kawaida.
Msemaji wa Shirika la Ndege la Pakistan amekaririwa na CNN akieleza kuwa wamejihakikishia abiria aliyefungua mlango huo wa dharura hakuwa na nia ovu bali alidhani ni mlango wa chooni. Alieleza kuwa abiria wote wako salama.
Mei mwaka jana, abiria mmoja alikamatwa nchini China baada ya kufungua mlango wa dharura wa ndege wakati ikiwa haijaanza kuruka. Alihojiwa na kufunguliwa mashtaka ya kuhatarisha usalama wa ndege.
Hivi karibuni pia, abiria aliyetambulika kwa jina moja ‘Song’ alifungua mlango wa dharura wakati ndege ikiwa inatua.