Wakati Wizara ya Katiba na Sheria ikiingia rasmi katika ofisi zake mpya mjini Dodoma jana baada ya kuhamia mwishoni mwa wiki, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi nayo imetangaza kuhamia mjini humo wiki mbili zijazo, huku ikiwatoa hofu watumishi wanaohamia huko kwa kuwataka kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo Mifugo na Uvuvi Mathew Mtigumwe, amewatoa hofu watumishi wa wizara yake kuwa suala la kuhamia Dodoma kuwa litafuata misingi na stahili za watumishi kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma.
Ameyasema hayo wakati wa kikao maalumu kilicholenga kujadili kwa pamoja namna ya utendaji kazi katika wizara hiyo sambamba na kutoa utaratibu utakavyokuwa kuelekea kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma.
Amesema awamu ya kwanza ya uhamisho utahusisha watumishi 88 kutoka Idara Kuu ya Mazao, watumishi 41 watahamia Dodoma kuanzia Februari 14 na 15, mwaka huu huku wengine 47 watahamia muda wowote kati ya mwezi huu na Juni mwaka huu.
Aidha, Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Harrison Mwakyembe amezindua rasmi ofisi za wizara yake Dodoma na kuwataka watumishi waliohamia kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Hilo limekuja mara baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kutoa mwelekeo wa kuhamia makao makuu ya nchi kwa Mawaziri kwamba ifikapo Februari 28, mwaka huu, tayari wizara kadhaa ziwe zimehamia Dodoma ikiwemo ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora iliyohamia wiki iliyopita.