Dakika chache baada ya kutangaza kumuondoa Anne Kilango Malecela katika nafasi ya Ukuu wa Mkoa wa Shinyanga siku 22 tu baada ya kumuapisha, Rais John Magufuli ametoa onyo kwa Mawaziri na Makatibu wakuu aliowateua.

Akizungumza leo Ikulu jijini Dar es Salaam, Rais Magufuli ameeleza kuwa anafahamu wapo baadhi ya mawaziri na Makatibu wakuu ambao wamekuwa wakilalamika ‘chinichini’ kuhusu upatikanaji mdogo wa fedha zinazoelekezwa katika matumizi mengine, yaani OC (Other Charges).

Amemtaka Katibu Mkuu Kiongozi kuwaonya Makatibu Wakuu wanaoanza kulalamika na kudai waongezewe OC na kwamba kama kuna anayeona fedha zinazotengwa ni chache ajiondoe.

“Chief Secretary, huo ndio muelekeo kwa Makatibu Wakuu wengine, waache kudai OC… ninawasikia. Wapo wanaodai OC ni chache, wakiona ni chache waache kazi. Wenzao wabunge wanasema ni nyingi,” alisema.

Rais Magufuli amesema kuwa ametuma watu waweze kuwarekodi mawaziri ambao wanalalamika ‘chinichini’ kuhusu OC akieleza kuwa watu hao bado wanadhani wako kwenye mfumo uliopita.

“Kuna mpaka Mawaziri wengine naona wanalalamika, nawatafutatafuta… nimetuma watu wawarekodi kwa sababu mind set yao bado haijabadilika. Wanafikiri bado tuko kwenye treni hiyohiyo. They will go,” Rasi Magufuli alisema kwa msisitizo.

Awali, Rais Magufuli alitangaza kutengua uteuzi wa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anne Kilango Malecela kutokana na kutoa taarifa kuwa hakuna mfanyakazi hewa kwenye Mkoa wake wakati timu ya Ikulu ilibainia uwepo wa wafanyakazi hewa 45 katika awamu ya kwanza ya ukaguzi.

 

Haji Duni akosoa Muundo wa Chadema
Maimartha amtolea uvivu Ray C