Mtu mmoja, anayedaiwa kutaka kuwauza watoto wake watatu wenye ualbino kwa kiasi cha Dola 40,000, ili kuwatumia katika tambiko la kishirikina, amekamatwa na vyombo vya usalama kabla ya kufanikisha jaribio hilo.
Msemaji wa Jeshi la Polisi katika eneo la Tete, lililopo kaskazini-magharibi mwa nchi ya Msumbiji, Feliciano da Camara amesema, watoto hao watatu (6-16), waliokolewa baada ya wasamaria wema kutoa taarifa kituoni.
Katika tukio hilo, pia mjomba wa watoto hao alikamatwa pamoja na baba yao, baada ya wawili hao kudaiwa kupanga kuwasafirisha watoto hao hadi nchi jirani ya Malawi ambako wangeweza kuuzwa kwa dola 40,000 au zaidi.
Hata hivyo, watuhumiwa hao wote wawili wanakana kuhusika katika kesi hiyo, huku msemaji huyo wa Polisi akisema, “Uchunguzi ulifanyika na iliwezekana kuwaokoa watoto wote watatu katika jaribio hilo.”
Baadhi ya nchi za Afrika za Kusini mwa Jangwa la Sahara, zimekumbwa na wimbi la mashambulizi dhidi ya watu wenye ualbino, ambao viungo vyao hutafutwa kwa ajili ya shughuli za kishirikina kwa imani kwamba vinaleta bahati na mali.
Juni 27, 2022, Mahakama nchini Malawi ilimhukumu kasisi wa Kikatoliki, Thomas Muhosha kifungo cha miaka 30 sambamba na watu wengine wanne kupata kifungo cha maisha kutokana na mauaji ya mwaka 2018 ya mwanamume mwenye ualbino.
Katika kesi hiyo, Jaji, Dorothy Nyakaunda Kamanga alisema Kasisi huyo aliyekuwa akiongoza parokia ya Machinga, kilomita 100 kaskazini mashariki mwa Blantyre, alikuwa na mpango wa kusafirisha viungo vya MacDonald Masambuka (22).