Baba Mzazi wa Kiungo wa Young Africans Salum Abubakar ‘Sure Boy’ amemtakia kila la kheri mwanawe kuelekea mchezo wa kesho Jumamosi (April 30) dhidi ya Simba SC.
Abubakar Salum baba mzazi wa Kiungo huyo amesema, ni furaha kwake kuona mwanawe amekua sehemu ya kikosi cha Young Africans kinachojiandaa na mchezo huo, lakini amesisitiza kuwa bado suala la kucheza ama kutokucheza anamwachia Kocha Nabi.
Amesema kama mzazi anamuombea Mwanawe aweze kuwa sehemu ya kikosi kitakachoanza dhidi ya Simba SC, ili aweze kuweka rekodi ya kucheza mchezo huo mkubwa akiwa amevaa jezi ya Young Africans.
“Ninamuombea kwa M.Mungu ili aweze kucheza mchezo wa kesho Jumamosi, lakini nafahamu maamuzi ya mwisho yapo kwa Kocha Nabi ambaye anajua nani anapaswa kuanza kwenye kikosi chake.”
“Ninamshauri mwanangu, kama atabahatika kuwa sehemu ya kikosi cha Young Africans kitakachoanza kesho Jumamosi, atambue mchezo huo ni mkubwa lakini hauna tofauti na michezo mingine kwa misingi ya sheria za soka na kupambana.”
“Anachotakiwa ni kutuliza akili yake na kuisaidia Young Africans kupata ushindi, nafahamu haitakua mara ya kwanza kwake kucheza dhidi ya Simba SC, amewahi kufanya hivyo akiwa Azam FC, hivyo kinachobadilika hapa ni jina la timu tu.” amesema mzee huyo ambaye pia aliwahi kuitumikia Young Africans.
‘Sure Boy’ alisajiliwa Young Africans wakati wa dirisha dogo la usajili akitokea Azam FC, na tayari ameshaonyesha uwezo mkubwa akiwa na kikosi cha Wananchi, hivyo huenda kocha Nabi akamtumia katika mchezo wa kesho dhidi ya Simba SC.
Young Africans kesho itaingia Uwanja wa Benjamin Mkapa huku ikiwa inaongoza msimamo wa Ligi Kuu kwa kufikisha alama 54 ambazo zinawapa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu 2021/22.
Simba SC inayotetea ubingwa inashika nafasi ya pili kwenye msimamo huo, ikiwa na alama 41, ambazo zinaifanya kuwa nyuma kwa alama 13 dhidi ya Young Africans.