Kampuni ya Bangi Inc iliyo chini ya Mathew Knowles ambaye ni baba mzazi wa mwanamuziki Beyonce imepanga kufanya biashara ya bangi jijini Nairobi nchini Kenya, endapo nchi hiyo itahalalisha matumizi ya mmea huo.

Mzee Mathew pamoja na wajumbe wa kampuni ya Bangi Inc wanaiangalia Kenya kama sehemu muhimu ya soko lao, wakiamini kuwa nchi hiyo itapitisha sheria itakayowapa nafasi ya kutengeneza pesa kupitia bangi.

Kampuni hiyo iliyosajiliwa Marekani, ilitangaza Agosti 7, 2019 kuwa Bodi yake ya Wakurugenzi imepitisha azimio ambalo litaifanya kuwa kampuni ya kwanza kuorodheshwa kwenye Masoko ya Hisa ya Nairobi na Marekani.

Mzee Knowles atakuwa na jukumu la kusimamia kampuni hiyo katika masuala ya matangazo, mawasiliano, ubunifu pamoja na matumizi ya mitandao ya kijamii.

“Kenya ni soko linalokuwa haraka katika miaka ya hivi karibuni, soko hili litavutia uwekezaji wa mabilioni ya dola za kimarekani,” Mtendaji mkuu wa Bangi Inc amekaririwa na Yahoo.

Hata hivyo, ingawa kumekuwa na mjadala kuhusu kuruhusu matumizi ya bangi nchini Kenya, bado sheria ya nchi hiyo kama ilivyo kwa nchi zingine za Afrika Mashariki inapiga marufuku matumizi ya mmea huo kwa namna yoyote. Bangi au marijuana imewekwa kwenye orodha ya dawa za kulevya katika nchi zote za Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Mzee Mathew alikuwa msimamizi wa kazi za mwanaye Beyonce kwa muda mrefu, lakini Machi 2011 mwanaye huyo alitangaza kumuachisha kazi.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Agosti 15, 2019
Abiria 47 wanusurika kifo