WAKATI kikosi cha Young Africans ikiwa kwenye maandalizi ya mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Tanzania Prisons, kocha wa zamani wa timu hiyo ya Wananchi, Hans van der Pluijm amefichua vile alivyompika nyota wa sasa wa kikosi hicho, Deus Kaseke.
Kaseke ni miongoni mwa wachezaji hatari kwenye kikosi cha Young Africans, ubora wake ulianza kuonekana Novemba 25 kwenye uwanja wa Azam Complex, Chamazi dhidi ya Azam, alifanya kibarua cha kocha wa timu hiyo, Aristica Cioba kuota nyasi, amekuwa wamoto tangu hapo.
Kwenye michezo sita ya ligi tangu alipoanza kuonyesha vitu vyake ameipachikia Young Africans mabao manne na hakuna mchezo ambao Wananchi wamedondosha pointi wakiwa na nyota huyo kwenye ubora wake na ndio kwanza idadi ya mabao imekuwa ikiongezeka tofauti na awali.
Pluijm ambaye ameifundisha Young Africans kwa awamu mbili tofauti, alisema Kaseke wakati akitokea Mbeya City, 2015 na kumtengeneza namna alivyopenda kumtumia.
“Najisikia vizuri kuona bado yupo kwenye kiwango kile kile, kuna mambo ambayo nilifanyia naye kazi kwa muda mrefu, nilipenda acheze mpira rahisi, kikubwa ilikuwa kukaa kwenye nafasi akiwa kama mchezaji huru,” alisema kocha huyo raia wa Uholanzi na kuongeza kuwa.
“Kiukweli hakuwahi kuvunjika moyo hata pale ambapo alikuwa akikosea nilipenda kumtia moyo lakini baadaye akaona wepesi wa namna ya kucheza mpira wa kisasa, alimudu kucheza pembeni, kati ya uwanja na hata kama namba 10 na ndio maana hata baada ya kuondoka Young Africans na kupata nafasi Singida nilitamani kufanya naye kazi,” alisema.
Baada ya kufanya kazi na Kaseke kwa miaka miwili Young Africans na baadaye kufungashiwa virago vyake na kuibukia Singida United, Pluijm hakuwa na muda wa kujiuliza katika mipango yake ya kuijenga timu imara aliona kuna uhitaji wa kuwa naye kikosini nyota huyo.
Pluijm anaonekana bado kuwa na kumbukumbu licha ya sasa kuwa na umri wa miaka 71, alisema alimsajili Kaseke Julai ya mwaka 2017 na kuwa mmoja wa wachezaji ambao walichangia mafanikio yake akiwa na Singida United, “Naamini ataendelea kuisaidia Young Africans na Tanzania kwa ujumla kama watajua namna nzuri ya kumtumia,” alisema.