Wasanii Wakongwe wa muziki wa dansi nchini, Nguza Viking maarufu kama Babu Seya na mwanaye, Johnson Nguza ‘ Papii Kocha’ leo January 5, 2018 wamepata ofa kabambe ya kurekodi muziki wao katika Studio za wanene Entertainment zilizopo Mwenge Dar es salaam.

Ofa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Juliana Shonza na mmiliki wa Studio hiyo ya  wanene Entertainment, Dash.

Ambapo Shonza leo amezungumza na waandishi wa habari amesema kuwa wizara yake ina dhamana na tasnia ya muziki hivyo kwa dhati imeamua kuwasaidia wasani hao ambao walipata msamaha wa Rais kutoka kifungoni ambapo walihukumiwa kifungo cha maisha jela.

” Sisi kama Wizara tumeamua kuendeleza vipaji vya Wasanii hawa ambao sisi ndio walezi wao, hivyo nimewasiliana na uongozi wa Wanene ambao wamekubali kushirikiana na sisi lengo ni kuhakikisha ubora wa hawa wasanii unarejea na wanafanya kazi” Alisema Shonza.

Nae Mmiliki wa Wanene, Dash amesema wameamua kwa dhati kuwasaidia wasanii hao.

Kwa upande wake Nguza Viking ‘ Babu Seya aliishukuru Serikali kupitia kwa Naibu Waziri na kuahidi kufanya kazi kama ambavyo Sera ya Rais Magufuli ya hapa Kazi Tu inavyosema na huku akijitamba kurudisha imani ya mashabiki wa muziki wa Dansi.

” Kwa sasa hatuwezi kusema tutarekodi ngoma ngapi lakini tunamshukuru Waziri na Dash kwa sapoti yao, sisi tunachowaahidi ni kufanya kazi kwa bidii kama Rais anavyotaka.

” Mimi ni msanii naweza kufanya aina yoyote ya muziki haijalishi ni wa aina gani, hivyo mashabiki wetu wakae mkao wa kula tumerudi kuwapa burudani,” alisema Papii Kocha.

Video: Kangi Lugola afunguka kuhusu mke wake
Trump akivuruga kitabu kinachomkosoa