Baada ya kusaini mkataba mpya ambao utaendelea kumuweka young Africans hadi mwaka 2027, Beki kutoka visiwani Zanzibar Ibrahim Hamad ‘Bacca’ amewaambia Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo, wajiandae kuona ubora zaidi kutoka kwake kuanzia kesho Jumamosi (Desemba 02) dhidi ya Al Ahly kwani kwa sasa ana mzuka wa aina yake.
Bacca alijiunga na Young Africans wakati wa Dirisha Dogo la usajili msimu wa 2021/22 akitokea KMKM ya Zanzibar, baada ya kuonyesha kiwango kizuri kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2022 na mwanzoni mwa juma hili klabu ilimuongezea mkataba wa miwili huku mchezo ujao dhidi ya Al Ahly umepewa jina lake ili kuhamasisha Mashabiki na Wanachama.
Amesema kucheza pamoja na manahodha wake Dickson Job na Bakari Mwamnyeto amekuwa akijifunza mengi na kuongeza na ujuzi alionao, na hiyo ndio siri ya kuaminiwana kupewa mkataba mpya.
Bacca amesema sio rahisi kuaminiwa na Young Africans, lakini yeye kapata hiyo nafasi tena kwa muda mfupi, hivyo ameahidi kupambana kuhakikisha anakuwa mmoja wa wachezaji watakaokumbukwa kwenye historia ya klabu hiyo, kama ilivyokuwa kwa wachache waliomtangulia.
“Kuongezwa mkataba wa muda mrefu ndani ya klabu kubwa ambayo ina ushindani mkubwa kwenye eneo ninalocheza kutokana na kuwa na wachezaji wazuri kunanipa nguvu ya kupambana na kuwapa kile wanachotarajia kutoka kwangu,” amesema Bacca na kuongeza;
“Ubora waliouona na kuniamini, naahidi sitawaangusha nitapambana kuhakikisha napata nafasi ya kuutumikia mkataba wangu kwa kuvuja jasho uwanjani na kuipa timu matokeo.”
Bacca amesema ubora wake unatokana na ushirikiano mzuri na wachezaji wenzake na amekuwa mwepesi wa kujifunza kuliko kujiona amekua kutokana na kupata nafasi, hivyo anawashukuru wachezaji wenzake kwa kumpa muongozo.
“Nimewakuta wamekuwa viongozi wangu kwenye uchezaji ninawashukuru wote, nimepata nafasi ya kucheza nao wana mchango mkubwa kwenye ukuaji wa kipaji changu nitaendelea kujifunza na kuwa miongoni mwa wachezaji watakaoipeleka timu pale wanapotamani kufika,”
“Nina deni kubwa kwa wanayanga kwa mkataba huu mpya sitawaangusha nitaendeleza pale nilipo na kuwa bora zaidi, lengo ni kuona nautumikia mkataba kikamilifu kwa kuvuja jasho.” amesema Bacca.
Amesema huwa wanakumbushana majukumu bila kujali ukubwa na uzoefu ndio kitu kinachowafanya wawe bora eneo la nyuma ya timu hiyo.