Nahodha na Beki wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans, Bakari Mwamnnyeto ameweka wazi kuwa wamekaa kikao cha wachezaji na kukubaliana kwa pamoja kuwa ni lazima wapate ushindi dhidi ya Al Merrikh ya Sudan ili wafikie malengo.
Young Africans itavaana na Al Merreikh katika hatua ya Kwanza ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika. Mchezo huo unatarajiwa kupigwa kesho Jumamosi (Septemba 30) kwenye Uwanja wa Azam Compex jijini Dar es salaam.
Akizungumza jijini Dar es salaam, Mwamnyeto amesema kuwa mashabiki wajitokeze kwa wingi kwa ajili ya kuwapa sapoti itakayowawezesha kuipambania timu.
Mwamnyeto amesema kuwa kila mchezaji amepanga kutimiza malengo yake kwa kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji.
Ameongeza kuwa wamepanga kupata ushindi mkubwa zaidi walioupata katika mchezo wa kwanza wa ugenini Rwanda.
“Mashabiki waondoe hofu kabisa ya ushindi, kama wachezaji tumefanya kikao na kukubaliana kuwa ni lazima kila mmoja aipambanie timu kwa dakika atakazocheza.”
“Hivyo mashabiki waondoe hofu kabisa, hivyo wajitokeze kwa wingi kutusapoti tutakapokuwepo uwanjani tukiipambania timu yao.” amesema Mwamnyeto.