Baraza Kuu la Waislaam Tanzania (Bakwata) limeliomba Jeshi la Polisi nchini kumkamata mtu mmoja anayejitangaza kuwa ni Mtume katika eneo la Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza jana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa Bakwata, Sheikh Khamis Mattaka (katikati pichani) alimtaja mtu huyo kwa jina la Hamza Issa, akieleza kuwa amekuwa akitoa mafundisho yaliyo kinyume na dini ya Kiislam na kufanya vurugu katika eneo la Misugusugu.
Sheikh Mattaka alisema kuwa mtu huyo ambaye hujiita Nabii Ilyasa anaweza kusababisha machafuko kwani amekuwa akitoa mahubiri potovu na kufanya fujo kwa kutumia vibaya dini.
Alisema kuwa kitendo cha kujitangaza kuwa yeye ni Mtume kinaweza kusababisha machafuko endapo hatadhibitiwa.
“Kudai kuwa yeye ni Mtume ni upotoshaji ambao ukiachwa unaweza kusababisha vurugu,” alisema Sheikh Mattaka.
Akizungumza wakati wa ibada ya sikuu ya Eid al-Fitr mwaka huu jijini Dar es Salaam, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakary Zubeir alikemea utoaji wa mafundisho potofu kuhusu dini ya kiislam. Mufti Zubeir alisema kuwa hakuna mafundisho ya dini ya kiislam yanayohamasisha vurugu au uvunjifu wa amani dhidi ya mtu yoyote akionya wanaofanya hivyo kuacha mara moja.