Mshambuliaji Mpya wa Simba SC Jean Othos Baleke amefunguka kwa mara ya kwanza kuhusu mipango na mikakati ya kuisaidia klabu hiyo katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.
Simba SC itashiriki Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika kuanzia mwezi Februari, ikipangwa Kundi C sambamba na Mabingwa wa Uganda Vipers SC, Horoya AC (Guinea) na Raja Casablanca (Morocco).
Baleke aliyesajiliwa Simba SC wakati wa Dirisha Dogo akitokea TP Mazembe ya DR Congo, amesema dhamira yake kubwa ni kuisaidia klabu hiyo kufikia malengo yake ya kutinga Nusu Fainali na ikiwezekana Fainali na kutwaa Ubingwa wa Afrika.
Amesema kabla ya kutua klabuni hapo, alizungumza na viongozi wa Simba SC na walimueleza matamanio yao ya kutaka kuiona klabu hiyo ikifanya vizuri zaidi kwenye michuano ya Kimataifa.
“Kwenye Michuano ya Kimataifa ndio kiu kubwa kwangu kuhakikisha nafanya vizuri kwa faida ya malengo makubwa ya timu, Simba SC kupitia viongozi wake tayari nimezungumza nao na malengo makubwa wamenieleza kuwa kiu yao ni kutaka kuona tunafanya vizuri katika Michuano hii.”
“Kwangu malengo yangu ni kuona naisaidia Simba SC kufanya vizuri katika Michuano hiyo mikubwa ambapo na mimi ni sehemu yangu ya kihakikisha naonekana ili niweze kuwa sehemu ya kikosi cha Timu ya Taifa ya DR Congo.” amesema Baleke
Tayari Baleke ameshaitumikia Simba SC katika mchezo mmoja wa Ligi Kuu dhidi ya Dodoma Jiji FC uliopigwa Jumapili (Januari 22) Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma.
Mshambuliaji huyo aliifungia Simba SC bao la ushindi na kuiwezesha Klabu hiyo kufikisha alama 53 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikitanguliwa na Young Africans yenye alama 56.