Kocha Mkuu wa Simba SC Roberto Oliveira Gonçalves do Carm ‘Robertinho’ amefanya kikao kizito na mastaa wake akiwemo Jean Baleke, lengo ni kumtaka kila mmoja kujitafakari na kujua ukubwa wa majukumu yaliyopo mbele yake, yanavyohitaji umakini na kujituma, ili kuipa thamani klabu hiyo.
Kikao hicho kimefanyika baada ya mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos uliopigwa Jumamosi (Septemba 16) na alichosisitiza kocha ni kuhakikisha hawarudii makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo.
Kocha Robertinho ametaka kila mchezaji ajitafakari kwa nafasi yake, kujua jinsi ya kuhakikisha timu inafanya vizuri, hasa katika kipindi hiki ambacho kila shabiki na mwanachama anataka kuwa na furaha.
Kocha huyo kutoka Brazil amesema: “Tulipata nafasi si chini ya saba, lakini tumezitumia mbili tu, ndio maana nasisitiza umakini ukiongezeka tutakuwa tunafunga mabao mengi zaidi na tutafanya makubwa, nimefanya kikao na wachezaji wote akiwemo huyo Baleke unayesema, huwa sipendi kuongelea mchezaji mmoja mmoja kwa kuwa naamini tunacheza kama timu.”
Amesema bado anakiamini kikosi chake, kina mastaa wenye uwezo mkubwa wa kuamua kila mechi, anachokifanya ni kukumbushana ili kuhakikisha wanafunga mabao mengi na wanaozuia wahakikishe golini kwao kunakuwa salama.
“Nataka kuona tunarekebisha makosa kwenye michezo ijayo ndio maana tunazungumza mara kwa mara kuwekana sawa.”
Simba SC hadi sasa msimu huu imefanikiwa kucheza mechi tano za mashindano yote, Ngao ya Jamii mbili dhidi ya Singida Fountain Gate na Young Africans ndani ya dakika 90 hiyo michezo haikupata bao, licha ya kunyakua ngao kwa njia ya Penati.
Michezo mingine ni ule wa Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ilishinda mabao 4-2 Uwanja wa Manungu na Dodomna Jiji ikishinda mabao 2-0 Uwanja wa Uhuru na mechi ya CAF dhidi ya Power Dynamos ikitoka sare ya mabao 2-2 Zambia.
“Ndio maana nimesema nina kikosi kizuri, ila nasisitiza umakini ukiongezeka utafanya timu ishinde mabao mengi na eneo la ulinzi kulinda vyema lango.
Simba SC itarudiana na Dynamos Oktoba Mosi kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na kama ikivuka itakwenda hatua ya makundi.
Baleke alikosa mabao mengi katika mchezo huo ulikuwa wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.