Mshambuliaji kutoka DR Congo Jean Baleke, ameahidi kujirekebisha na kuisaidia timu yake ya Simba SC katika mchezo wa Mkondo wa Pili wa kuwania kufuzu Hatua ya Makundi Ligi ya Mabingwa Barani Afrika dhidi ya Power Dynamos ya Zambia.
Baleke alikosa mabao mengi katika mchezo wa Mkondo wa Kwanza uliopigwa Jumamosi (Septemba 16) katika Uwanja wa Levy Mwanawasa ambao ulimalizika kwa sare ya 2-2.
Mshambuliaji huyo amesema atarekebisha makosa yake kwa kuhakikisha anafunga mabao yatakayoisaidia Simba SC kutinga Hatua ya Makundi katika mchezo wa Mkondo wa Pili uliopangwa kupigwa Oktoba Mosi, mwaka huu, huku akiwaomba Wanachama na Mashabiki kujitokeza kwa wingi Uwanja wa Azam Complex, Dar es salaam.
Beleke amekiri kukosa mabao ambayo yangeweza kuifanya Simba SC kuibuka na ushindi, lakini akasema yote hayo yamepita na anaangalia mechi ya marudiano ambayo Simba itacheza nyumbani, akiahidi kufunga idadi kubwa ya mabao kwenye mguu wake ili kuwafurahisha na kuwapoza wanachama na mashabiki wa timu hiyo.
“Hii imeisha, tunaangalia mechi ya nyumbani, hapa nyumbani tutawafunga mabao mengi, na mimi nitafunga mabao mengi mechi ya marudiano,” amesema Baleke.
Amesema matokeo ya sare ya mabao 2-2 waliyoyapata ugenini ni mazuri na kwa sasa wana matumaini makubwa ya kwenda hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mara nyingine tena msimu huu.
“Baada ya sare hii matumaini ni makubwa ya sisi kuingia makundi, nawaomba tu wanachama na mashabiki waje kwa wingi uwanjani kwa ajili ya kutupa sapoti, sisi tutawafurahisha pia.” amesema.