BALOZI wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Mh. Richard Lupembe, ameweka wazi kuwa Azam FC ni moja ya timu zinazowatia moyo kama Watanzania wanoishi nje ya nchi, huku akiipa mkono wa ushindi kuelekea mchezo wa marudiano dhidi ya Mbabane Swallows ya Afrika Kusini.
Lupembe alitoa kauli hiyo wakati alipoitembelea timu hiyo jana kwenye kambi yake katika Hoteli ya Acardia jijini Pretoria, nchini humo ikijiandaa na mchezo huo wa Kombe la Shirikisho Afrika utakaofanyika Uwanja wa Taifa wa Somhlolo nchini Swaziland Jumapili hii saa 10.30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
“Kwa kweli nimefarijika sana kwa kuiona Azam FC tena kama nakumbuka mlikuja hapa mwaka jana, mlikuja hapa kucheza (vs Bidvest) na nikawa mgeni rasmi na mkono wangu ukawa wa kheri mkashinda, nawahakikishieni nitawashika tena mkono na ninauhakika mtashinda tena,” alisema Lupembe wakati akizungumza na mtandao wa klabu www.azamfc.co.tz
Alisema kuwa atakuwa pamoja na timu hiyo kwa kipindi chote itakapokuwa jijini hapa hadi Jumamosi itakapoelekea Swaziland huku akiitakia kila la kheri kuelekea mtanange huo unaosubiriwa na mashabiki wengi wa timu hizo.
“Ndio tunafahamu kuwa kuna timu kubwa za Simba na Yanga, lakini Azam FC inatia moyo kwa sisi watu ambao tulioko nje nawatakia kila la kheri, mazoezi mema mimi nipo hapa kama balozi, na nitahakikisha nitakuwa na nyie mpaka siku mtakapoenda kucheza mpira,” alisema,
Lupembe aliitembelea Azam FC jioni wakati ikielekea kwenye mazoezi kujiandaa na mchezo huo.
Mara mwisho Balozi huyo kuishika mkono Azam FC iliichapa Bidvest Wits mabao 3-0 jijini Johannesburg katika mchezo wa raundi kama hii, ambapo kutokana na ushindi wa 1-0 katika mchezo wa kwanza kwa sasa timu hiyo inahitaji ushindi wowote au sare ili iweze kusonga mbele.