Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Mwenyekiti wa Kamati ya Maafisa Waandamizi wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Balozi Kanali Wilbert Ibuge amefungua kikao cha Maafisa Waandamizi chenye jukumu la kundaa ajenda za mkutano wa Baraza la Mawaziri utakaofanyika tarehe 18, Machi mwaka huu Jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mkutano huo ambao unafanyika kwa ‘Video Conference’, Balozi Ibuge amesema kuwa kikao hicho kitajadili ajenda mbalimbali zikiwemo Taarifa ya Maandalizi ya Dira ya SADC ya mwaka 2050, Mpango Mkakati wa Maendeleo wa SADC 2020-2030, Maadhimisho ya miaka 40 ya SADC tangu kuanzishwa kwake mwaka 1980, Utekelezaji wa maazimio ya vikao vilivyopita, Hali ya michango ya kifedha kwa ujumla ya SADC pamoja na Kupokea taarifa ya ukaguzi wa shughuli mbalimbali za Sekretariati ya SADC.
“Kikao hiki kinafanyika kwa njia ya ‘Video Conference’ kufuatia ushauri uliotolewa na Mawaziri wa Afya wa Nchi za SADC walipofanya Mkutano wa dharura kufuatia mlipuko wa Ugonjwa wa Virusi vya Corona (Covid-19), uliofanyika Jijini Dar es Salaam Machi 9, 2020 na tutakuwa na ajenda chache, nawasihi tuendelee kufuatilia na kutekeleza yale yote ambayo tumeyaazimia”, amesema Balozi Ibuge.
Pamoja na hayo, Balozi Ibuge amebainisha kuwa kuna uwezekano wa Maafisa Waandamizi wa Nchi hizo za ukanda wa Kusini Mwa Afrika (SADC), kukutana mwezi Juni 2020 iwapo hali ya sasa ya mlipuko wa ugonjwa wa Corona (Covid-19, itakuwa imebadilika ili kujadili kwa kina ajenda zilizosalia na nyingine zitakazopendekezwa.
Mkutano huo ambao umeendeshwa kwa mara ya kwanza kwa kutumia njia ya Mtandao yaani ‘Video conference’ kwa nchi za SADC, umethibitisha kukua kwa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA)-ICT na itaendelea kuimarishwa zaidi kwa Nchi hizi ili kuepuka kuwepo kwa taharuki ya milipuko mbalimbali au adha ambazo zitasababisha kuahirishwa kwa mikutano hiyo.
Aidha, balozi Ibuge amewataka wananchi wanachama kuendelea kuchukua tahadhari kujikinga na ugonjwa wa Corona ili kuepusha kusambaa katika nchi wanachama.
Naomba nitumie fursa hii kuwaomba na kuwasihi nchi wanachama kuendelea kujikinga na maambukizi ya Covid-19 na kushikamana kwa umoja wetu kupunguza kasi ya maambukizi na hatimaye kuondoa kabisa katika sura ya dunia”, Amesema Balozi Ibuge.