Mkuu wa Itifaki wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Kanali Wilbert A. Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na mabalozi mbalimbali wanaowakilisha nchi zao hapa nchini pamoja na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa.
Mazungumzo hayo yamefanyika kwa siku mbili, tarehe 22 na 23 Januari 2020 katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya Tanzania na nchi hizo na mashirika hayo.
Mabalozi hao ni Balozi wa Visiwa vya Comoro, Mhe. Balozi Ahamada Elbadaour Mohamed, Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Balozi Frederic Clavie, Balozi wa Denmark nchini Mhe. Balozi Mette Norgaard na Balozi wa Iran nchini, Mhe. Balozi Mousa Farhang, Balozi wa Ethipia nchini, Mhe. Balozi Yonas Yosef Sanbe, pamoja na Balozi wa Italia nchini, Mhe. Balozi Roberto Mengoni.
Mbali na mabalozi, Mkuu wa Itifaki, Balozi Kanali Ibuge amekutana na Wakuu wa Mashirika ya Kimataifa ambao ni Naibu Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto (UNICEF) Bw. James Gitau na Mwakilishi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Aga Khan (AKDN) Bw. Amin Kurji.