Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amewataka mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani kuongeza jitihada za kuhakikisha Diplomasia ya Uchumi inaleta tija iliyokusudiwa.

Balozi Ibuge ametoa kauli hiyo wakati alipokutana na kufanya mazungumzo kwa nyakati tofauti na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe, Prof. Emmanuel Mbennah pamoja na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Wilson Masilingi katika Ofisi ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.

Balozi Ibuge katika mazungumzo yake na Balozi wa Tanzania nchini Zimbambwe Prof. Mbennah amemtaka kuhakikisha kuwa anafanya kazi kwa weledi katika kuimarisha uhusiano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Jamhuri ya Zimbabwe pamoja na kukuza diplomasia ya uchumi kwa kuzingatia maelekezo ya Serikali. 

“Balozi nakusihi kuendelea kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kufanikisha azma na malengo ya Serikali katika kuhakikisha tunaimarisha uhusiano wetu wa kidiplomasia na Zimbabwe lakini pia kukuza diplomasia ya Uchumi kati yetu na Zimbabwe,” amesema Balozi Ibuge.

Kwa upande wake, Balozi Prof. Mbennah amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa uhusiano wa Jamhuri ya Muungano na Tanzania na Zimbabwe ni mzuri na imara.

Katika tukio jingine, Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Brigedia Jenerali Wilbert Ibuge amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Marekani Wilson Masilingi ambapo pamoja na mambo mengine wamejadili umuhimu wa kuhakikisha kuwa Tanzania inanufaika ipasavyo na uhusiano mzuri wa kidiplomasia ilionao na Marekani.

Naye Balozi Masilingi amemhakikishia Katibu Mkuu kuwa Ubalozi wa Tanzania nchini Marekani unaendelea kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa kasi inayotakiwa. 

CORONA: CAF yafanya mabadiliko
Tanzania kunufaika na Bilioni 8 kwa ajili ya migebuka