Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amekutana na kuzungumza na Jumuiya ya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania – FEMATA, waliofanya ziara ya siku 12 yenye lengo la kutafuta wawekezaji, kujifunza Teknolojia na kuboresha Mahusiano mema ya kibiashara inayohusisha zaidi ya Wadau milioni sita Nchini.
Akizungumza katika Mkutano hivi karibuni, Balozi Kairuki amesema hiyo ni kati ya ziara nane zilizofanyika Nchini humo ndani ya miaka sita, mbili zikihusu sekta ya Madini na ya sasa amepewa heshima ya kipekee ya kuagwa na kuongozana na Uwakilishi wa Serikali, ambao uliwakilishwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Msafiri Mbibo.
Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwaaga baada ya kupata Uteuzi wa kituo kipya cha kazi Nchini Uingereza, na kuwahikikishia kuwa Balozi mpya ajaye ni Mtu makini na anaufahamu wa Biashara hivyo ana uhakika yaliyoanzishwa yataendelezwa huku akiwasihi Wafanyabiashara wauze bidhaa kuliko malighafi na kuwatoa wito kwa Mabenki kuwakopesha Wafanyabiashara wa Madini ili kukuza sekta husika.
Naye Rais wa FEMATA, Bina ameishukuru Serikali na kumuhakikishia Balozi Kairuki kuwa wataendeleza ushirikiano na china, na watakutana na Balozi mpya wa China, Omar ili kujenga Mahusiano na kuendeleza manufaa ya ziara waliyofanya.
Amesema ziara hiyo imewapa mafunzo, uwezo mkubwa wa kuboresha Sekta ya Madini Tanzania,kufanya biashara kwa urahisi kati ya Nchi mbili , kuboresha Mahusiano kwa kuanzisha Ofisi ndogo ya FEMATA Nchini China na kuingia makubaliano mbalimbali yenye lengo la kuiinua sekta ya madini Nchini.