Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Balozi Liberata Mulamula amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi jijini Dakar nchini Senegal.
Katika mazungumzo yao viongozi hao wameelezea kuridhishwa kwao na ushirikiano na uhusiano imara uliopo kati ya Tanzania na China na kuahidi kuendeleza uhusiano huo kwa faida ya pande zote mbili.
Waziri Mulamula amemuhakikishia Waziri Yi utayari wa Serikali kuendelea kushirikiana na China katika kuhakikisha Tanzania inafikia maendeleo ya kweli kwa ufanisi mkubwa.
Amemshukuru Waziri huyo kutokana na ahadi iliyotolewa awali na Rais Xi Jinping wa China wakati wa ufunguzi wa mkutano wa FOCAC ya kutoa dozi bilioni moja zaidi za chanjo ya virusi vya Covid 19 kwa bara la Afrika kwani kitendo hicho kitazisaidia nchi za Afrika kutoa chanjo ya ugonjwa huo kwa watu wengi zaidi.
Pia ameishukuru China kwa kuwa soko la bidhaa za Tanzania na amemuhakikishia Waziri huyo kuwa Tanzania iko tayari kutumia fursa ya soko la China la kuuza mazao yake ya mbogamboga na matunda ili kuongeza ujazo wa biashara na hivyo kukuza uchumi.
Naye Waziri Yi kwa upande wake ameishukuru Tanzania kwa kuendelea kuiunga mkono China na kuahidi kuendelea na harakati za kusaidia nchi zinazoendelea na kuongeza kuwa China itaendelea kuisadia Tanzania katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati na kuielezea Reli ya TAZARA kama moja ya kielelezo cha ushirikiano huo.
Mawaziri hao wako Senegal kuhudhuria Mkutano wa Nane wa Mawaziri wa Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) unaofanyika nchini Senegal ulioanza tarehe 29 hadi 30 Novemba 2021.