Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano na Afrika Mashariki, Balozi Liberata Mulamula ameomba radhi wale ambao hawakumuelewa kwa kutotosikika vizuri alipokuwa akiwasilisha mapendekezo ya bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki kwa mwaka wa fedha 2021/ 2022.

Balozi Mulamula ameomba radhi wakati wa kipindi cha mahojiano kilichofanyika kituo cha habari cha ITV jana Juni 15, 2021.

“Kupitia fursa mlionipatia niombe radhi kwa wale ambao waliona kwamba..ile speed niliwaangusha hawakusikia hata kile nilichokuwa nasema” Liberata Mulamula – Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,” amesema Balozi Mulamula.

“Kama ulivyosema Wizara yetu ina mambo mengi sana, unapewa muda mfupi, kwa mfano kama sisi Wizara ya Mambo ya Nje mambo yetu ni mtambuka, lakini nina balozi 43, zote zile taarifa ipo kwenye ile bajeti, mango lazima ‘u-cover’ maeneo yote yale, kwa hiyo ndo maana watu waliona ile speed…. Pale spika aliposema una dakika 5, halafu nilikuwa nina page (kurasa)  kama kumi,” amefafanua Balozi Mulamula.

Mapema mwezi huu wakati akiwasilisha makadirio ya bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022, Waziri Mulamula alisikika akizungumza kwa haraka na kutokumalizia kutamka baadhi ya maneno hivyo wengi kushindwa kuelewa alichokuwa anakiwasilisha.

Waziri Mulamula aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2021/22, jumla ya Shilingi Bilioni 192.2 ambapo kati ya hizo bilioni 178.7 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na bilioni 13.5 ni kwa ajili ya bajeti ya maendeleo.

Balozi Mulamula aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Aprili Mwaka huu wakati Rais Samia Suluhu Hassan alipofanya mabadiko ya Baraza la Mawaziri.

Manispaa ya Ubungo yaja na mkakati huu kuwaondoa wanaolala daraja la Kijazi
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Juni 15, 2021