Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amaesema ujio wa Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika James Duddridge hapa nchini unadhibitisha mahusiano mazuri ya Tanzania nje ya mipaka yake licha ya taarifa potofu zilizokuwa zikisambaa katika mitandao ya kijamii na vyombo vya habari vya nje zikitilia mashaka juu ya diplomasia ya Tanzania nje ya nchi.

Waziri Mulamula amesema kuwa ziara hiyo ni kielelezo cha Tanzania kuheshimika na kukubalika miongoni mwa Jumuiya za Kimataifa na Mataifa ya nje na kwamba kipaumbele cha Serikali ya awamu ya sita ni diplomasia ya uchumi ambapo Uingereza ni moja kati ya nchi tatu kubwa zinazowekeza hapa nchini na hivyo kuwa ni miongoni mwa Mataifa muhimu kwa Tanzania

Balozi Mulamula ameongeza kuwa katika mazungumzo yao msisitizo mkubwa umewekwa katika uchumi na kukuza biashara pamoja na kuiendeleza miradi mikubwa iliyokuwa ikitekelezwa na Uingereza ikiwemo miradi ya kiwanda cha sukari na madini. 

Aidha, amemuhakikishia James Duddiridge kuwa mazingira ya uwekezaji ni salama na yanavutia baada ya kuboreshwa na hivyo kumtaka kuwahamasisha wawekezaji kutoka Uingereza kuja hapa nchini kuwekeza katika sekta mbalimbali. 

Naye, Waziri wa Uingereza anayeshughulikia masuala ya Afrika James Duddridge amesema Uingereza na Tanzania ni mbia muhimu wa miaka mingi wa maendeleo na katika Jumuiya ya Madola na kwamba Nchi ya Uingereza itaendelea kushirikiana na Tanzaniakatika masuala ya uwekezaji,biashara,diplomasia na utawala bora.

Aidha, Duddridge ameongeza kuwa ziara yake ya siku mbili hapa nchini ina lengo la kuendelea kuimarisha mahusiano baina ya Uingereza na Tanzania licha ya changamoto ya ugonjwa wa COVID – 19 ambapo Uingereza imekusudia kuisaidia Tanzania kuboresha mifumo ya ukusanyaji kodi,mapambano dhidi ya rushwa lakini pia katika sekta za Afya na Elimu.

 

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Mei 12, 2021
Rais Samia aifumua Mahakama, DPP achomolewa