Uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki umesikitishwa na kifo cha Balozi wa Tanzania nchini Austria na Mwakilishi wa Kudumu katika Ofisi ya Umoja wa Mataifa, Vienna, Celestine J. Mushy aliyefariki kwa ajali ya gari iliyotokea Mkata, Handeni Mkoani Tanga Desemba 13, 2022.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, imeeleza kuwa Balozi Mushy amefariki baada ya gari aliyokuwa akisafiria kutoka Dar es Salaam kuelekea Mkoani Kilimanjaro kugongana na lori la mizigo na hatimaye kuungua moto na yeye akiwa ndani yake.
Ukandamizaji: Wanahabari 533 wafungwa jela
Taarifa hiyo imebainisha kuwa, ”Wakati wa uhai wake ameitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika nafasi mbalimbali zikiwemo Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimataifa katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kaimu Katibu Binafsi wa Waziri Mkuu katika Serikali ya Awamu ya Nne na Katibu Tawala Msaidizi wa Masuala ya Uchumi, Sektetariet ya Mkoa wa Mtwara.”
Balozi Mushy atakumbukwa kwa umahiri wake mkubwa katika masuala ya kidiplomasia, ambapo Wizara kwa kushirikiana na familia ya Marehemu inaendelea na mipango ya maandalizi ya mazishi na itakapokamilika wananchi watajulishwa na inatoa pole kwa familia.