Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), Balozi Seif Ali Iddi ameonyeshwa na kutembelea eneo ambalo zitajengwa Ofisi za Serikali hiyo eneo la Mahoma Makulu Jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kutembelea eneo hilo, Balozi Iddi ambaye aliambatana na Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar, Balozi Amina Salum Ali ameishukuru Serikali kwa kupewa eneo hilo.
Aidha, ameahidi kuwa SMZ itaanza ujenzi wa Ofisi zake katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha na kama watapata fungu ujenzi utaanza mapema iwezekanavyo ili waweze kuhamia katika Makao Makuu ya Nchi.
Katika ziara hiyo ujumbe kutoka Zanzibar ulipokelewa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Balozi Joseph Sokoine, Kaimu Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu Ofis hiyo, Samuel Mwashambwa na viongozi mbalimbali.
Akizungumza kuhusu eneo hilo Mratibu wa Mchakato wa Kuhamishia Serikali Dodoma kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Meshack Bandawe amesema kuwa eneo hilo lina ekari 30.
Hata hivyo, ameongeza kuwa tangu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli alipotangaza Serikali kuhamia Makao Makuu ya Nchi Julai 25, 2016 ulianzishwa mchakato wa kuhamisha watumishi.