Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Iddi ameitaka Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TANTRADE) kuendelea kuimarisha mitandao na mifumo ya biashara nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara wa Tanzania kuweza kuwa na uhakika wa masoko bora ya bidhaa za ndani na nje ya nchi.

Balozi Idd amesema kuwa Maonyesho hayo ya mwaka huu yameonyesha dhamira na mwelekeo wa Serikali katika kutumia fursa ya biashara na viwanda katika kujenga uchumi imara pamoja na kutengeneza ajira kwa wananchi.

Amesema kuwa ni wajibu wa TANTRADE kutumia fursa za uwepo wa makampuni ya wazalishaji, wauzaji na wafanyabiashara kutoka nje wanaoshiriki katika maonyesho hayo kuweza kujenga mitandao imara ya mahusiano na ushirikiano kwa wafanyabiashara wa ndani ili kuweza kuwatafutia masoko ya bidhaa zao ambazo kwasasa zimeanza kuzalishwa katika viwango bora nchini.

“Nawapongeza TANTRADE kwa juhudi zenu za kuanzia klinilki za biashara, na hili limewezesha wafanyabiashara wetu kuweza kukutana na wanunuzi mbalimbali ambao huweza kuwapa uzoefu wa namna bora zaidi ya kuzalisha bidhaa zenye kukidhi viwango na ubora unaotakiwa,”amesema Balozi Iddi.

Aidha, Balozi Iddi amesema kuwa Serikali kwa sasa inatekeleza Mpango Kazi wa Kuboresha Mfumo Udhibiti wa Biashara Nchini (Blue Print), ambao umekusudia kuondoa changamoto mbalimbali za wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi, hivyo ameitaka TANTRADE kushirikiana na wadau na wazalishaji wa sekta binafsi ili kuiwezesha sekta ya biashara kuvutia wawekezaji wengi zaidi.

Kwa mujibu wa Balozi Iddi pia ameitaka TANTRADE kuweka utaratibu wa kufuatilia oda za maombi mbalimbali zinazotolewa na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi ili kuendelea kupanua wigo wa soko la bidhaa za Tanzania nje ya nchi ambalo kwa sasa limeendelea kupanuka kutokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali.

Hata hivyo, ameongeza kuwa maonyesho hayo ya 43 yamethibitisha uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania katika kutengeneza na kuzalisha bidhaa mbalimbali kwani idadi ya washirki wa maonesho kutoka nje ya nchi imeweza kuongezeka kutoka makampuni kutoka nje 2956 mwaka 2018 hadi kufikia 3250 mwaka 2019, hivyo kudhibitisha uwezo wa serikali katika kusimamia sekta ya biashara nchini.

Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa amesema kuwa Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara nchini ikiwemo kuanza kufanya mapitio ya sera na sheria mbalimbali ambazo awali zilikuwa zikileta changamoto mbalimbali kwa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi.

 

Wakulima wa kilimo cha umwagiliaji wapewa somo
Wanaobet wapewa saa 48 kuondoa pesa zao la sivyo zinachukuliwa #Kenya