Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza imemuita balozi wa China jijini London, Liu Xiaoming kutoa maelezo kuhusu kuongezeka kwa hali ya wasi wasi wa Kidiplomasia uliosababisha na maandamano makubwa ya kuipinga China, Hong Kong, ambalo lilikuwa koloni la zamani la Uingereza.
Liu Xiaoming ameitwa kujibu maswali juu ya kile wizara ya mambo ya nje ya Uingereza ilichosema kuwa ni matamshi yasiyokubalika na yasiyo sahihi kutoka China juu ya Hong Kong.
Aidha, balozi huyo wa China amemtuhumu waziri wa mambo ya nje wa Uingereza, Jeremy Hunt, kwa kuunga mkono kile alichosema kuwa ni watu wanaofanya ghasia na wavunja sheria na kuituhumu pia Uingereza kwa kuendelea kuwa na fikira za kikoloni kuelekea jimbo hilo.
Serikali ya Uingereza mara kadhaa imeahidi uungaji mkono mamia kwa maelfu ya waandamanaji huko Hong Kong, ambao wamefanya maandamano makubwa katika wiki za hivi karibuni kuelezea hasira zao kwa serikali inayoungwa mkono na China.
Hata hivyo, waandamanaji pamoja na Uingereza wameilaumu China kwa kukiuka msingi wa mfumo wa nchi moja mifumo miwili iliyoahidiwa kutekelezwa wakati Uingereza ikikabidhi jimbo hilo kwa China mwaka 1997, wakisema serikali ya mji huo inayounga mkono China inazidi kuwa ya kimabavu na inamilikiwa na China.