Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula (Mb) amepokea nakala ya Hati za Utambulisho kutoka kwa Balozi Mteule wa Ethiopia nchini Shibru Mamo Kedida leo katika Ofisi Ndogo za Wizara Jijini Dar es Salaam.
Baada ya kupokea nakala ya hati hizo viongozi hao walipata fursa ya kuzungumza ambapo Balozi Mulamula alimhakikishia Balozi Mteule ushirikiano wa hali ya juu kumuwezesha Balozi huyo kutekeleza majukumu yake ya kibalozi hapa nchini na kuhakikisha uhusiano kati ya Tanzania na Ethiopia unaendelea kuimarika.
‘‘Unaona timu yangu niliyoambatana nayo hapa, nichukue nafasi hii kukuhakikishia kuwa Wizara itakupa ushirikiano wote utakaouhitaji katika kutekeleza majukumu yako, saa 24 milango yetu iko wazi, tunataka uhusiano kati ya nchi zetu uzidi kuimarika,’’ alisema Balozi Mulamula.
Balozi Mulamula amesema Tanzania imefarijika kupata balozi mpya baada ya Balozi wa awali kumaliza muda wake wa uwakilishi, na kuongeza kuwa kitendo hicho ni ishara ya uhusiano mzuri na urafiki uliopo baina ya Tanzania na Ethiopia.
Naye Balozi Mteule wa Ethiopia Sibru Mamo Kedida amemshukuru Waziri Mulamula kwa jinsi alivyompokea na kuelezea uhusiano kati ya Tanzania na Ethiopia ulivo mzuri na kuahidi kuwa atahakikisha uhusiano huo unazidi kukua na kuimarika.
“Ethiopia na Tanzania zimekuwa katika uhusiano mzuri sana kidiplomasia, nchi zetu zimekuwa na lengo moja, nitahakikisha uhusiano kati ya nchi hizi unaimarika na hata kufikia nchi hizi Tanzania na Ethiopia zinashirikiana kufanya biashara na uwekezaji kwa maslahi ya pande mbili,” amesema Balozi Kedida.