Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Umoja wa Falme za Kiarabu – UAE, Lt. Jen. Mstaafu Yacoub Hassan Mohamed amewasilisha Hati za Utambulisho kwa Rais wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Sheikh Mohammed Bin Zayed Al Nahyan katika Ikulu ya nchi hiyo, iliyopo jijini Abu Dhabi.

Akizungumza baada ya kupokea hati hizo, Rais Al Nahyan alimuhakikishia ushirikiano na Serikali yake katika kutekeleza majukumu nchini UAE kwa manufaa ya pande zote mbili huku Balozi Mohamed akimuahidi Rais kuwa atahakikisha Watanzania na Waemirati wananufaika na fursa za kiuchumi zilizopo.

Nchi hizo mbili zina fursa nyingi za kushirikiana kiuchumi hususan katika sekta ya nishati ambayo UAE ni miongoni mwa nchi tajiri katika uzalishaji wa mafuta huku Tanzania ikiwa na eneo kubwa la kilimo hivyo ina soko kubwa la bidhaa za Kilimo na Mifugo ambapo ushirikiano huo utawezesha uzalishaji wa kisasa na kuongeza thamani ya bidhaa.

Bidhaa zenye soko kubwa kwa Tanzania nchini UAE ni mbogamboga, matunda, nyama, korosho, karafuu, chai, karanga, asali, samaki na kahawa na pamoja na Umoja wa Falme za Kiarabu, ubalozi huo pia unawakilisha nchi za Bahrain, Pakistan na Iran.

Wachezaji Ligi Kuu waonywa utovu wa nidhamu
Neymar afichua sababu ya kutimkia umangani