Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera amepiga marufuku kwa muda safari za nje kwa Serikali yake na yeye mwenyewe, ili kuisaidia nchi yake kupunguza matumizi katika kukabiliana na mzozo wa kiuchumi.
Hatua ya Chakwera ambaye ni Muhubiri wa zamani wa Kiinjilisti, inatoa taswira kuwa sasa hataenda kwenye mkutano wa kilele wa tabianchi wa COP28, uliopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi wa Novemba 2023 katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Amesema, “Natangazwa kusitishwa kwa safari zote za nje zinazofadhiliwa na Serikali kwa maafisa wa ngazi zote hadi mwisho wa mwaka wa fedha mwezi Machi, wajumbe wote wa serikali waliopo safari za kikazi nje ya nchi waharakishe kurejea nyumbani, pia nusu ya bajeti ya mafuta ya Maafisa Wakuu wa Serikali imepunguzwa.”
Mapema wiki hii, Malawi ilitangaza kushuka kwa thamani ya asilimia 44 ya sarafu yake ya Kwacha, ili kuweza kupata mkopo wa IMF na Taifa hilo limetatizwa kwa miongo kadhaa wa kufikia ukuaji endelevu wa kiuchumi licha ya kupokea bajeti kubwa za misaada ya maendeleo.