Beki wa Richardsbay FC au Natal Rich Boys, Mtanzania Abdi Banda ameshinda kesi aliyoifungua dhidi ya timu yake ya zamani Chippa United ambayo sasa inatakiwa kumlipa Randi 4.5 milioni (sawa na Sh 600 milioni).
Kupitia mwanasheria wake, Lyrique de Plessis raia wa Uingereza, Banda alifungua kesi FIFA kudai mkataba wake baada ya Chippa kuuvunja kinyume cha sheria.
Banda aliingia kwenye mgogoro na klabu baada ya kuitwa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ Mei, mwaka huu ambapo Chippa ilimtaka kupunguza mshahara kuanzia Juni Mosi jambo ambalo alilikataa.
Akizungumza na kwa njia ya simu kutoka Afrika Kusini, Banda amesema kukataa kupunguza mshahara ni sababu ya waajiri wake kusitisha mkataba na kuamua kukimbilia FIFA.
“Mwanasheria wangu alifungua mashtaka FIFA na alihakikisha anapambana napata haki zangu baada ya kuona mkataba ulivunjwa kimakosa, tayari hukumu imetoka ikitaka Chippa inilipe stahiki zangu. Nimefurahi sana kwa hilo,” amesema.
“Chippa sikuwahi kukaa nao chini kukubaliana ili mshahara wangu upunguzwe zaidi ya wao kutuma barua iliyoelekeza hivyo. Halikuwa jambo jepesi kwangu, huenda linawapata na wachezaji wengi.”
Baada ya kushtaki na kabla ya kutoa hukumu, FIFA iliitaka Chippa iwasilishe barua ya utetezi kuhusu kesi hiyo Julai 18, huku hukumu yenyewe ilitarajiwa kutolewa Septemba 18, ila imewahi zaidi.