Kiungo kutoka DR Congo Yannick Bangala amefurahishwa na kiwango cha Feisal Salum Abdallah ‘Fei Toto’ akisema jamaa ameanza kuwa mtamu huku akimpa ushauri juu ya mashabiki wanaomzomea kwenye mechi zao.
Fei alionyesha kiwango cha hali ya juu Jumatatu (Oktoba 23) wakati timu yake ya Azam FC ilipopoteza kwa kuchapwa mabao 3-2 na Young Africans kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Bangala ambaye alikuwa akicheza pamoja na Fei Toto wakati wakiwa Young Africans na sasa wapo wote Azam FC, amesema kiungo huyo ameanza kurudi kwenye kiwango chake lakini anatakiwa kuwapuuza mashabiki wanaomzomea.
Bangala amesema Fei Toto anatakiwa kuendelea kupambana uwanjani bila kuyaingiza kichwani makelele ya mashabiki hao kama ambavyo alifanya mchezo uliopita walipokutana na Young Africans.
Amesema endapo Fei Toto ataendeleza kiwango hiki alichonacho sasa atawanyamazisha wote ambao wamekuwa wanaomzomea.
“Ukiangalia alivyofika hapa Azam FC na alivyo sasa hasa alipocheza mechi dhidi ya Young Africans utaona jinsi anavyoimarika, alicheza kwa kiwango kikubwa ni kwa kuwa tulipoteza mechi ile lakini ujumbe umefika,”amesema Bangala.
“Najua anakutana na ugumu kwa watu wanaomzomea mimi namshauri awapuuze asiweke makelele yao kichwani kwake akiendelea na kiwango hiki atawafanya wanyamaze,”
Fei Toto tangu ahame Young Africans mashabiki wa timu hiyo wamekuwa wakimuandama kwa kumzomea kila mchezo, lakini ameonekana kuwa makini na kazi yake zaidi.
Kiungo huyo ni mmoja kati ya wale wenye mabao mengi kwenye Ligi Kuu Bara akiwa ameshapachika mabao manne hadi sasa.