Klabu ya Simba kupitia Idara ya Habari na Mawasilino inayoongozwa na Ally Shantri ‘Chico’ wamegoma kufanya kikao cha Kocha na Waandishi wa Habari kwa kushinikiza kuondolewa kwa Bango lenye nembo ya GSM.
Mkutano wa Makocha kwa ajili ya mchezo wa kesho Jumamosi (Desemba 11) wa Simba na Young Africans ulikuwa unafanyika leo Ijumaa (Desemba 10) katika makao makuu ya Shirikisho la Soka nchini (TFF).
Kocha wa Young Africans, Nassredine Nabi ndiye aliyeanza kuzungumza na alipomaliza msemaji wa TFF, Clifford Ndimbo aliwataka Simba SC waingie lakini waligoma.
Chico alisikika akisema ”Toeni bango kwanza”.
Baada ya Simba SC kugoma kuingia Ndimbo aliwaruhusu wadhamini wakuu wa Ligi, NBC kuingia na kuzungumzia mchezo huo.
Ikumbukwe tangu juma lililopita Simba waliandika barua ya kuomba ufafanuzi juu ya udhamini wa TFF na GSM walioingia na kutaka nembo ya kampuni hiyo kuwa sehemu ya jezi.
Kabla ya kugomea kufanya Mkutano na Waandishi wa Habari, Magari mawili ya Simba SC aina ya Harrier (Rabi Hume) na Mercedes Benz (Chico na Pablo Franco) yaliingia katika ofisi za TFF.