Mshambuliaji Umaru Bangura ametajwa kwenye kikosi cha Sierra Leone, ambacho kitaanza mchakato wa kusaka nafasi ya kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2021) kuanzia juma lijalo.
Sierra Leone wataanza mchakato huo, kwa kukutana uso kwa macho na Lesotho Novemba 13, na siku tatu baadae watapambana dhidi ya Benin.
Bangura, ambaye kwa sasa anawatumikia mabingwa wa zamani wa Uswiz FC Zurich, alikua njia panda kufanya maamuzi ya kulitumikia taifa lake, kufuatia purukushani zilizojitokeza kati yake na mashabiki wa nchi hiyo mjini Freetown mwezi Septemba.
Mashabiki wa soka wa Sierra Leone waliingia katika matatizo na mshambuliaji huyo, baada ya kuchukizwa na hatua ya kukosa mkwaju wa penati wakati wa mchezo wa kuwania kufuzu fainali za dunia 2022, dhidi ya Liberia, ambao walifanikiwa kutinga hatua ya makundi, kwa ushindi wa jumla wa mabao matatu kwa mawili.
Mashabiki wenye hasira walifikia hatua ya kuvamia nyumbani kwa mshambuliaji huyo mjini Freetown na kufanya fujo, huku wakiamini penati aliokosa Umaru Bangura ingeisaidia Sierra leone kufuzu kucheza michezo ya hatua ya makundi kombe la dunia 2022, ukanda wa barani Afrika.
“Nimeamua kuendelea kulitumikia taifa langu, baada ya kuzungumza na wanafamilia, wameniomba kurejesha moyo wangu wa kizalendo, pia nimezungumza na viongozi wa chama cha soka Sierra Leone pamoja na baadhi ya viongozi wa serikali,” Alisema mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 33.
“Ninalipenda sana taifa langu, japo nilikwazika na kilichotokea baina yangu na mashabiki, lakini nimeamua kusamehe na kuangalia namna ya kuisaidia timu yangu ya taifa ili iweze kufuzu fainali za Afrika (AFCON 2021).”
Wachezaji wengine walioitwa kikosini na kocha raia wa Ghana Sellas Tetteh upande wa makipa yupo Solomon Zombo Morris (Tolouse Rodeo, France) na John Tyre (Scarborough SC, Canada)
Mabeki: Mustapha Dumbuya (Phoenix Rising, USA) Hassan Sesay (HIFK, Finland), Ali Sesay (Arda Kadzali, Bulgaria) na Umaru Bangura (FC Zurich) Usman Kakay (Patrick Thistle, Scotland)
Viungo; John Kamara (Keshla FC, Azerbaijan), Kwame Quee (Vikingur, Iceland), Ibrahim Conteh (Pursipura, Indonesia) na Abdul Sesay (OLS, Finland).
Washambuliaji: Mohamed Buya Turay (Djurgarden, Sweden), George Kweku Davies (St. Pultin, Austria), Kei Kamara (Colarado Rapids, USA) na Mustapha Bundu (Aarhus GF, Denmark).