Bao la kwanza lililofungwa jana na beki wa kati Henock Inonga, limeingia kwenye rekodi ya mabao ya haraka kufungwa kwenye Kariakoo Derby, akifuata nyayo za Emmanuel Okwi aliyefanya hivyo mwaka 2012.
Simba SC na Young Africans zilivaana jana Jumapili (April 16) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam katika pambano la 110 la Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965 na Wekundu kuibuka na ushindi wa mabao, huku Inonga akiitanguliza kwa bao la dakika 1 na sekunde 43.
Beki huyo kutoka DR Congo alifunga bao hilo kwa kichwa akimalizia krosi ya Shomary Kapombe aliyeanzishiwa kona fupi na Inonga kuruka hewani mbele ya mabeki wa Young Africans na kumtungua kipa Djigui Diarra.
Beki huyo anakuwa beki wa kati wa pili wa Simba SC kufunga kwenye Derby kwa miaka ya karibuni baada ya Joash Onyango aliyefunga kwenye pambano la Novemba 07, 2020 ambalo liliisha kwa sare ya 1-1, beki huyo Mkenya akichomoa bao la Young Africans lililowekwa kimiani na Michael Sarpong.
Tangu mwaka 2012, bao la Okwi lililofungwa kwenye pambano la watani lililpigwa Mei 6 na Simba SC kushinda mabao 5-0, ndilo lililokuwa la mapema zaidi, akifunga dakika ya kwanza.