Mwenyekiti wa Kamati Ndogo ya Hamasa Haji Manara, amewataka mashabiki wa soka kuhakikisha wanafika Uwanja wa Taifa Novemba 15, kwa ajili ya kuishangilia Taifa Stars itakayokua na mtihani wa kupambana na Equatorial Guinea kuanzia Saa 1:00 usiku, kama walivyofanya katika michezo iliyopita.
Manara amesema anajua jukumu kubwa lipo kwa waandishi wahabari kufikisha ujumbe wa kamati yake, lakini bado anaamini mashabiki nao watafikishiana habari kila kukicha ili kufikia lengo linalokusudiwa.
Pia akayataka makampuni nchini kujenga utamaduni wa kununua tiketi za mchezo wa soka ili kufanikisha lengo la kuwasaidia mashabiki ambao hawajiwezi kufika uwanja wa taifa la kuishangilia timu yao.
Katika hatua nyingine Haji Manara amewaomba Watanzania kujitokeza kwa wingi katika mchezo huo, ili kuutumia kama pongezi kwa nahodha Mbwana Samatta na kikosi kiujumla.
Manara amesema ipo haja kwa watanzania kurejesha heshima kwa Samatta kwa kufika uwanjani siku hiyo ya Novemba 15, kwa ajili ya kumshangilia sambamba na wachezaji wenzake wa Taifa Stars.
“Jana Samatta amefanya jambo kubwa na la kipekee kwa kufunga bao kwenye Uwanja wa Anfield dhidi ya Liverpool. Ni vyema tukajitokeza kwa wingi iwe ishara ya kumpongeza kwa kile alichokifanya.
“Tangu timu yetu ya taifa ilipofuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (Chan) hatujapata nafasi ya kuwapongeza kama nchi hivyo tuutumie mchezo wetu dhidi ya Equatorial Guinea kutimiza hilo,” alisema Manara.
Mwenyekiti wa chama cha mashabiki wa soka Tanzania, Karigo Godson alisema hamasa ya mashabiki ina nafasi kubwa ya kuipa matokeo chanya Stars.
“Mashabiki tunapojitokeza kwa wingi na kuwashangilia vijana wetu, wanapata hamasa na kujituma zaidi,” alisema Karigo.