Bao la Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Senegal na klabu ya Simba SC Pappe Ousmane Sakho dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast limetangazwa kuwa bao Bora la Wiki ya kwanza ya Michuano ya Kombe la Shirikisho Hatua ya Makundi msimu huu 2021/22.
Simba SC iliwakaribisha ASEC Mimosas Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam Jumapili (Februari 13), katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza wa ‘Kundi D’ na kuibuka na ushindi wa mabao 3-1.
Sakho alifunga bao hilo kwa Tick Tack akiunganisha mpira uliokua umepigwa na Beki wa Pembeni Shomari Salum Kapombe dakika ya 12 kipindi cha kwanza.
Hii ni mara ya pili kwa Simba SC kupata fursa ya kuwa na bao Bora la Wiki lililofungwa na mchezaji wake katika mchezo wa kwanza Hatua ya Makundi uliochezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, baada ya kufanya hivyo msimu uliopita kwa bao la Kiungo Mshambuliaji kutoka Msumbiji Luis Miquissone akiifunga Al Ahly ya Misri.
Mchezo wa Simba dhidi ya Al Ahly ulikuwa wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu uliopita wa 2020/21, ambapo Mnyama alichomoza na ushindi wa bao moja kwa sifuri.
Mabao mengine ya Simba SC katika mchezo dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast uliopigwa Jumapili (Februari 13), yalifungwa na Beki wa kulia wa Tanzania Shomari Salum Kapombe kwa njia ya Penati dakika ya 79 na Kiungo Mshambuliaji kutoka Malawi Peter Banda dakika ya 81.
Kwa matokeo hayo Simba SC imepata alama tatu sawa na RS Berkane iliyoibamiza US Gendamarie mabao 5-3.