Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka Wananchi kutoa taarifa za hali ya ubovu wa miundombinu ya Barabara nchini kupitia mfumo wa Kieletroniki wa ‘Barabara App’ ili hatua za haraka ziweze kuchukuliwa kwa zile zinazohitaji matengenezo.
Bashungwa ameyasema hayo Septemba jijini Dodoma wakati akihitimisha ziara yake katika Bodi ya Mfuko wa Barabara – RFB, ambapo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo, ambapo Barabara App hiyo sasa itasaidia maeneo mengi kukarabatiwa kwa haraka na hivyo kuondokana na ajali zinazoweza kuzuilika.
Amesema, kupitia mfumo huo Wananchi wanaweza kusimamia miundombinu ya barabara katika maeneo wanayoishi au kupitia utumaji wa taarifa muhimu za hali ya barabara katika Bodi ya Mfuko wa Barabara – RFB, ambayo itawasilisha ujumbe kwa TANROADS na TARURA.
Aidha Waziri Bashungwa ameongeza kuwa miongoni mwa taarifa hizo ni zile za Barabara kujifunga, Daraja au Kalavati kubomoka/ kuzolewa na mafuriko, mashimo hatarishi Barabarani, kazi kufanyika chini ya kiwango, Mitaro kuziba na hujuma zozote zinazofanyika katika Miundombinu ya Barabara.