Baada ya kuanza vizuri msimu mpya wa ligi Kuu Tanzania Bara, kwa kuifunga Gwambia FC bao moja kwa sifuri, kocha mkuu wa Biashara United Mara Francis Baraza, amesema hana budi kuwashukuru wachezaji wake kwa kazi nzuri walioifanya.
Biashara United walianza vizuri msimu wa 2020/21 kwa kuibamiza Gwambia FC iliyopanda daraja ikitokea Ligi Daraja la kwanza, bao moja kwa sifuri na kujikusanyia alama tatu za awali.
Kocha Baraza amesema wachezaji wake walionyesha ukakamavu wakati wote wa mpabano huo uliochezezwa majira ya saa nane mchana Septemba 06, na anaamini hali hiyo itaendelea kwenye mchezo mingine msimu huu.
“Nawapongeza wachezaji wangu wamefanya kazi kubwa, wamefuata maelekezo ambayo niliwapa na yamewasaidia kupata alama zote tatu.” amesema Baraza.
Kocha huyo kutoka nchini Kenya amesema waliingia kwenye mchezo huo wa tahadhari kubwa kutokana na kuwa walicheza na timu ambayo ni ngeni kwenye Ligi Kuu.
Amesema wachezaji wake walitumia dakika 45 kuwasoma wachezaji wa timu ya Gwambina, na wakafanikiwa kupata ushindi huo.
“Tuliwasoma muda mrefu, wachezaji wangu walipowajua wakaweza kupata ushindi mzuri dakika za lala salama na ninaahidi kufanya vizuri zaidi kwenye mechi zinazofuata.”
Biashara United Mara watacheza mchezo wa mzunguuko wa pili wa Ligi Kuu kwa kucheza na Mwadui FC kwenye uwanja wa Karume, mjini Musoma-Mara.
Mwadui FC walipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya Dodoma Jiji FC, kwa kufungwa bao moja kwa sifuri, na watahitaji kupamabna vilivyo kwenye mtanange dhidi ya Biashara United Mara, ili kujipatia alama tatu muhimu.