Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa jana limechukua hatua ya nadra ya kuitisha mkutano wa dharura wa wanachama wote 193 wa Baraza Kuu la Umoja huo kujadili kuhusu azimio la kulaani uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.
Baada ya Urusi kutumia kura yake ya turufu kuzuia azimio hilo kwenye baraza la usalama wiki iliyopita sasa mataifa ya magharibi wana matumaini ya idadi kubwa ya wanachama kulaani uvamizi huo wa Urusi kwenye mkutano huo uliopangwa kufanyika baadae leo.
Balozi wa Uingereza kwenye Umoja wa Mataifa Barbara Woodward amesema Urusi haiwezi kuuzuia ulimwengu kuungana pamoja kulaani uvamizi huo.
Mkutano huu utakuwa wa 11 wa dharura wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa katika kipindi cha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake.
Kwa kuwa mataifa mengi yanatarajiwa kutoa hotuba, mkutano huo huenda ukadumu kwa siku saba.
Balozi wa Ufaransa kwenye Umoja huo Nicola De Riviere alitangaza kwamba baraza la usalama litafanya mkutano hii leo kuhusiana na athari za kibinaadamu kufuatia uvamizi huo, kikao kilichoombwa na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ili kuhakikisha ufikishwaji wa misaada kwa idadi inayoongezeka ya wale wenye mahitaji nchini Ukraine.