Baraza la habari la Kenya (MCK) limeipa New York Times saa 24 kufuta mara moja picha zinazoonesha miili ya wahanga wa shambulizi la kigaidi katika eneo la 14 Riverside jijini Nairobi.
Kupitia barua yake iliyotolewa jana, MCK wamelaani kitendo kilichofanywa na chombo hicho cha habari cha Marekani, ikikielezea kuwa ni kinyume na maadili, kukosa heshima na uchapishaji wenye kudhalilisha.
“MCK inapinga vikali sababu zilizotolewa na New York Times kuwa lengo la kuchapisha picha zinazoonesha miili ya wahanga wa shambulizi lilikuwa kuwaonesha wasomaji wake picha halisi ya tukio hilo baya,” imeeleza taarifa ya MCK.
Baraza hilo, mbali na kutoa saa 24 kwa chombo hicho cha habari chenye umaarufu mkubwa duniani, imekitaka kuomba radhi kupitia kurasa zake kwa kitendo hicho.
Barua hiyo imeeleza kuwa endapo New York Times haitafanyia kazi maelekezo hayo ya kiungwana, MCK watachukua hatua sitahiki haraka iwezekanavyo.
Ukomo wa siku iliyotolewa kwenye barua hiyo iliyosainiwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa MCK, David Omwoyo Omwoyo ni Januari 21 mwaka huu.
Wakenya walianza kulaani kitendo cha New York Times kuchapisha picha hizo kupitia mtandao wa Twitter na kuifanya kuwa gumzo, hali iliyovuta usikivu wa chombo hicho cha habari ambacho kilitoa majibu yake ambayo hata hivyo hayakuwaridhisha Wakenya na MCK.