Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi  (NEEC) lilianzishwa kupitia sheria ya Taifa ya uwezeshaji wananchi Kiuchumi  namba 16 ya mwaka 2004, ikiwa ni chombo cha juu cha kusimamia na kuratibu utekelezaji wa Sera ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Aidha, Baraza hilo la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ambalo lipo chini ya ofisi ya Waziri Mkuu,  linasimamia  mkakati wa Kitaifa wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi kupitia madawati ya uwezeshaji kuanzia ngazi ya Wizara , Idara, Taasisi, Mikoa na Halmashauri zote nchini.

Katika kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya vijijini, Serikali ya awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli iliahidi kutoa  Milioni 50 kwa kila kijiji kama fedha za Mfuko wa Mzunguko (Revolving  Fund) ili ziweze kuwasaidia wananchi kuboresha maisha yao.

Kadhalika, miongoni mwa malengo ya kuwakopesha vikundi vya wajasiliamali kupitia vyama vya ushirika vya akiba na mikopo (SACCOS) ni  kuwasaidia vijana katika  kuendeleza shughuli mbalimbali  za kiuchumi ambazo zitasaidia katika kujiletea maendeleo yao.

Hivi karibuni,  Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi Beng’i  Issa alisema kuwa kuna baadhi ya Taasisi au watu Binafsi ambao wanapita kuwadanganya wananchi kuwa mpango wa Shilingi Millioni 50 kwa ajili ya kila Kijiji zinapitia  kwenye Taasisi zao na kuwataka wananchi kuwa makini na watu wa namna hiyo.

Pia Beng’ alisema kuna baadhi ya taasisi ambazo zimekuwa zikiwatoza wananchi fedha katika viwango mbalimbali kwa kile wanachodai kuwa ni ada ya usajili ili vikundi hivyo vya wajasiliamali viweze kusajiliwa na kutambuliwa na hatamaye kufaidika na Mpango wa milioni 50.

Nionanvyo mimi,  NEEC kama chombo cha juu katika  kuwawezesha  wananchi kiuchumi ambacho pia  kipo kisheria, kina wajibu wa kusimamia na kuratibu   mpango mzima wa ahadi iliyotolewa na serikali kuhusu kila kijiji kupatiwa milioni 50.

Pamoja na kufuatilia mgawanyo huo wa Milioni 50 kwa kila kijiji lakini NEEC pia inawajibu wa kuhakikisha inawachukulia hatua za kisheria taasisi na wadau wote ambao wanapita kuwadanganya wananchi kuwa wametumwa na Baraza hilo jambo ambalo si la kweli.

Isitoshe NEEC pia linatakiwa kuwafahamisha wananchi kuhusu utaratibu mzima wa kuwafikia walengwa wa fedha hizo ili kuwaondolea usumbufu ambao unaweza kujitokeza  pindi serikali itakapokamilisha mpango wa ugawaji wa milioni 50 kwa kila kijiji.

Vilevile, Baraza hilo la Uwezeshaji wa Wananchi Kiuchumi (NEEC) linatakiwa kuvisimamia baadhi ya vyama vya ushirika vya akiba na mikopo ( SACCOS) ambavyo vinaonekana kutotumia vizuri fedha hizo ambapo malengo yake ni kuwasaidia wananchi kujikwamua katika hali ya umasikini.

Hata hivyo, katika kufanikisha mpango huo wa milioni 50 kwa kila kijiji, Baraza linatakiwa kuwaandaa wananchi kwani inaonekana baadhi yao hawana maandalizi mara watakapopata fedha hizo watawezaje kuzalisha baada ya mtaji.

Msukumo wa Serikali ya awamu ya tano wa kuwawezesha wananchi kiuchumi ni jambo jema na la kuungwa mkono na kila anayependa maendeleo katika nchi yetu na mwenye moyo wa uzalendo wa kujali hali za maisha za wananchi walio wengi.

Wakati wa Utawala wa awamu ya nne wa Rais Mstaafu Jakaya Kikwete ,Serikali ilitoa fedha za uwezeshaji maarufu kama mabilioni ya ‘JK’ ambapo hazikuweza kutumika vizuri kutokana na baadhi ya viongozi wa Saccos kudaiwa kutengeneza vikundi feki ili waweze kujikopesha fedha hizo.

Nape ataka wasanii hawa watengwe
Rais Magufuli Asaini Miswaada Mitano Kutumika Kama Sheria