Baada ya kupokea kisago cha mabao manne kwa sifuri kutoka kwa mabingwa watetezi Simba SC, kocha mkuu wa Biashara United Mara Francis Baraza ameweka wazi mapungufu yaliyopelekea kikosi chake kukubali kisago hicho.

Biashara United Mara wamepoteza mchezo wa kwanza msimu huu 2020/21 wakiwa nje ya mkoa wa Mara, baada ya kucheza michezo miwili ya Ligi Kuu na kujikusanyia alama sita na kufunga mabao mawili.

Kocha Baraza amesema kikosi chake kmekua na changamoto ya kupambana na kujiamini kinapocheza michezo ya ugenini, jambo ambalo analifanyia kazi, kwani kuna michezo mingine ya ugenini itakayowakabili siku za usoni.

Kuhusu kichapo cha mabao manne kwa sifuri walichokipata jana Jumapili, Septemba 20 kutoka kwa Wekundu Wa Msimbazi Simba, Baraza amesema walizidiwa mbinu ndani ya uwanja.

“Hamna tatizo ndani ya timu, wachezaji wamepambana kwa ajili ya kusaka matokeo ila mwisho wa siku tumepoteza kwa kuwa tulikuwa tumezidiwa mbinu.”

“Ninachokifanya kwa sasa ni kutafuta mechi nyingi zaidi za kirafiki ambazo tutacheza tukiwa ugenini hizo zitatuongeza hali ya kujiamini na kufanya vema zaidi.”

“Kwa hiki tulichokipata kinatuumiza lakini ni matokeo ndani ya uwanja. Tunakwenda kujipanga zaidi ili kurejea kwenye kasi yetu,” amesema.

Biashara United Mara inakua timu ya pili kufungwa mabao manne katika mchezo mmoja msimu huu, wakitanguliwa na Mbeya City walioambulia kisago kama hicho kutoka kwa KMC FC kwenye mchezo wa mzunguuko wa kwanza Jijini Dar es salaam.

Alexandre Lacazetti aombwa kuwa na SUBRA.
Manara ampongeza Yondan

Comments

comments