Afisa Mtendaji Mkuu wa klabu ya Simba SC Barbara Gonzalez, amewatoa hofu Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo kuhusu ushiriki wao kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Simba SC imepangwa kundi D sambamba na US Gendarmerie ya Niger, RS Berkane ya Morocco na Asec Mimosa ya Ivory Coast.

Barbara amesema Simba SC ipo tayari kushiriki michuano hiyo na Uongozi umejipanga ipasavyo ili kufanikisha malengo ya kutinga hatua ya Nusu Fainali na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa michuano hiyo.

“Tupo imara kwa namna ambavyo tunafanya hivyo mashabiki wasiwe na mashaka na sisi katika yale ambayo tunafanya, wachezaji wanajituma katika kutimiza majukumu yao.”

“Imani yetu ni kwamba tutafanya vizuri kwenye ligi na kwenye Kombe la Shirikisho, kwani haya nayo ni mashindano makubwa kimataifa kwa kuwa tupo kuiwakilisha nchi kimataifa, mashabiki wazidi kutuombea.”

Simba SC itaanzia nyumbani Februari 13 kwa kuikaribisha Asec Mimosa ya Ivory Coast, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, kisha itakwenda ugenini Niger kupambana na US Gendarmerie Februari 20 na Februari 27 itasafiri kuelekea Morocco kupambana na RS Berkane.

Machi 13 Simba SC itarejea Dar es salaam kucheza dhidi ya RS Berkane Uwanja wa Benjamin Mkapa huku mchezo unaofuata itacheza dhidi ya Asec Mimosa ugenini Machi 20 kabla ya kumaliza michezo ya hatua ya makundi kwa kuikaribisha US Gendarmerie Aprili 03.

Micho apiga panga The Cranes
Pawasa: Simba SC itapeta Kombe la Shirikisho