Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC, Barbara Gonzalez ametangulia Afrika Kusini, tayari kwa maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Rbo Fainali Kombe la Shirikiho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates.
Simba SC Jumapili (April 24) itacheza mchezo huo Uwanja wa Orlando, huku ikiwa na kibarua cha kulinda ushindi wake wa bao 1-0, ama kusaka ushindi zaidi, ili kutinga Hatu ya Nusu Fainali.
Akizungumza kutoka nchini Afrika Kusini Barbara amesema Uongozi wa Simba SC umedhamiria kuandaa mazingira mazuri kabla ya kuwasili kwa kikosi chao nchini humo, ili kuepuka usumbufu ambao huenda ukajitokeza.
Amesema lengo kuu la klabu hiyo ni kutaka kuona wachezaji wao wanakua sawa kisaikolojia kabla na wakati wa mchezo huo, utakaoanza saa kumi na mbili kwa saa za Afrika Kusini, sawa na Saa moja Usiku kwa saa za Tanzania.
Barbara pia amethibitisha kuwa, Kikosi cha Simba SC kitawasili Afrika Kusini siku moja kabla ya mchezo wake na Orlando Pirates (Jumamosi – April 23).
“Lengo letu Afrika Kusini ni moja tu ambalo ni kupata matokeo yatakayotufanya tufuzu nusu fainali. Tayari nipo hapa na timu itawasili Jumamosi siku moja kabla ya mchezo,”
“Simba SC imebadilika, inajua ugumu wa michezo ya ugenini lakini kila mmoja ndani ya timu yupo tayari kwa nafasi yake kuhakikisha tunatinga Nusu Fainali.”
“Tunajiamini tunakwenda kufanya vizuri, Kocha na Benchi la Ufundi kwa ujumla wanaendelea vizuri na maandalizi kwa morari ya juu kuhakikisha tunapata matokeo tunayoyahitaji kwenye mchezo wa marudiano, Jambo ambalo linawezekana kwani Simba SC imabadilika na inastahili kusonga mbele zaidi.” amesema Barbara.
Kikosi cha Simba SC tayari kimeshaanza maandalizi ya mchezo wa Mkondo wa Pili Hatua ya Robo Fainali tangu juzi Jumanne (April 20), Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo nje kidogo ya Jiji la Dar es salaam.