Afisa Mtendaji Mkuu wa Klabu ya Simba Barbara Gonzalez amesema amegundua ukubwa wa klabu ya Simba SC baada ya kufanya vizuri katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika kwa misimu mitatu iliopita.
Simba SC ilicheza hatua ya Robo Fainali ya Michuano hiyo msimu wa 2018/19 na kutolewa na TP Mazembe ya DR Congo huku msimu wa 2020/21 ikitolewa na Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Barbara amesema alipokwenda nchini Cameroon mwishoni mwa juma lililopita, alipata sifa nyingi za Klabu ya Simba SC kutoka kwa Maafisa wa Shirikisho la soka Barani Afrika ‘CAF’.
“Hivi karibuni nimerudi kutoka Cameroon, nilipokuwa kule na Mkurugenzi wa CAF tukiongelea Super League nimegundua kwamba Simba ni kubwa mno, Simba inapoongeleka kule ni kimataifa zaidi, tunapewa heshima kubwa mno.” Amesema Barbara
Simba SC msimu huu inashiriki Kombe la Shirikisho Barani Afrika baada ya kutolewa kwenye Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika na Jwaneng Galaxy ya Botswana.
Jumapili (Februari 13) Simba SC itaanza kampeni ya kusaka nafasi ya kucheza Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kuikabili ASEC Mimosas ya Ivory Coast katika mchezo wa ‘Kundi D’.
Timu nyingine zilizopangwa ‘Kundi D’ kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika ni RS Berkane ya Morocco na US Gendamarie ya Niger.