Afisa Mtendaji Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Barbara Gonzalez amesema hana shaka na mpango wa kikosi chao kutinga hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho, huku wakijiandaa kuelekea mchezo wa mwisho wa Kundi D dhidi ya USGN.
Jumapili (Machi 20) Simba SC ilipoteza dhidi ya ASEC Mimosas kwa kufungwa 3-0 nchini Benin, hatua ambayo iliifanya klabu hiyo yenye maskani yake jijini Dar es salaam kusubiri mchezo huo wa mwisho ili kufahamu hatma ya kutinga hatua ya Robo Fainali.
Simba SC itakua mwenyeji wa USGN kutoka Niger April 03 Uwanja wa Benjamin Mkapa mishale ya saa moja usiku, huku ikihitaji ushindi wa aina yoyote ili kujihakikishia nafasi ya kutinga Robo Fainali ya Michuano hiyo.
Barbara amesema Uongozi wa Simba SC unafahamu umuhimu wa mchezo huo wa mwisho, hivyo watakiandaa vyema kikosi chao ili kifanikishe azma ya kuibuka na ushindi kama ilivyokua katika michezo dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast iliyokubali kufungwa 3-1 na RS Berkane ya Morocco iliyolala 1-0 kwa Mkapa.
“Tunajua umuhimu wa mchezo wetu dhidi ya USGN, tutahakikisha tunafanya maandalizi ya kutosha kwa kila hatua ili kufikia lengo la kupata ushindi, Wachezaji wetu wanajua umuhimu wa mchezo huo na hata sisi viongozi tunajua hilo, hivyo Mashabiki wanapaswa kuwa pamoja na timu yao kuelekea mchezo huo muhimu.”
“Mashabiki wetu kazi yao ni moja kutuombea timu ifanye maandalizi vizuri, isitokee mchezaji yoyote akaumia na kushindwa kuwa sehemu ya mchezo siku ya mechi wajitokeze kwa wingi kulingana na nafasi ya kuingiza mashabiki tutakayopata na wote washangilie mwanzo mwisho tutafanikiwa kuweka rekodi nyingine ya kufuzu,” amesema Barbara.
Simba SC imefikisha alama 07 sawa na RS Berakane ya Morocco katika msimamo wa Kundi D, huku ASEC Mimosas ikiongoza kwa kuwa na alama 09 na USGN inaburuza mkia ikiwa na alama 05.
Wakati Simba SC ikicheza dhidi ya USGN Apri 03 Uwanja wa Benjamin Mkapa, ASEC Mimosas nayo itakua na kibarua kigumu cha kuikabili RS Berkane ugenini mjini Berkane-Morocco.